Bank ya CRDB Mkoani Katavi imetoa viti na meza sitini(60) kwa Shule ya Sekondari ya Wasichana Katavi iliyoko Wilayani Nsimbo Mkoani Katavi kwa lengo la kusaidia mkakati wa kukabiliana na upungufu wa samani katika shule hiyo, ikiwa mpango wa Benki hiyo kurudisha fadhila kwa jamii kutokana na faida inayopatikana katika miradi mbalimbali inayotekelezwa na benki hiyo.
Akikabidhi samani hizo kwa Jumuiya ya Shule ya Sekondari ya Wasichana Katavi, Meneja wa Benki ya CRDB kanda ya Nyanda za Juu Kusini Bi. Jenifer Tondi amesema kuwa Benki hiyo kupitia mkakati wake wa “Keti Ujifunze” itaendelea kushirikiana na serikali kuhudumia wananchi. Bi. Tondi ameongeza kuwa Pamoja na shughuli zake za kibenki, Benki hiyo inatenga asilimia moja ya faida yake ili kusaidia huduma mbalimbali katika jamii ikwemo afya, elimu na mazingira.
Akipokea Samani hizo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Mhemshimwa Jamila Yusuph ameishukuru Benki ya CRDB kwa jitihada zake za kuunga juhudi za maendeleo katika Mkoa wa Katavi na kuwaomba wadau wa maendeleo pamoja na wawekezaji wengine kujitokeza kuisaidia jamii kwa kadiri wanavyoapata katika kazi zao. Amesema kuwa serikali inafarijika sana hasa pale wadau wa maendeleo wanapojitokeza kuisaidia jamii.
Mheshimiwa Jamila Yusuph ametumia wasaa huo kuikumbusha jumuiya nzima ya shule hiyo kuzitunza miundombinu yote ya shule hiyo ikiwa ni Pamoja na samani walizokabidiwa ili ziweze kudumu na kutumiwa na vizazi vijavyo. Pamoja na hayo, Mkuu huyo wa Wilaya ameusihi uongozi wa shule hiyo kuimarisha ulinzi katika mazingira yote ya shule ili waishio wawe salama Pamoja na miundombinu yote iliyomo.
Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa Wilaya ya Mpanda Mheshimiwa Jamila Yusuph amewasihi walimu kuendelea kuwalea Watoto katika njia iliyo sahihi ili waweze kuyafikia malengo yao bila vikwazo. “Tunatambua sasa hivi zipo changamoto ya malezi hasa kwa Watoto wetu wanapotokea maeneo tofautitofauti, madam mmekebidhiwa jukumu hilo wanapokuwa shuleni mtusaidie kuwalea, kuwarekebisha lakini pia kuwasaidia waweze kufikia ndoto zao ……….”
Awali akitoa taarifa ya shule hiyo ya sekondari ya Wasichana Katavi, Mkuu wa Shule hiyo Bi. Elinesi Sossy Mwangomba aliainisha kuwa shule hiyo ina ufinyu wa ardhi hivyo kukosekana kwa viwanja vya michezo jambo linakosesha wanafunzi fursa ya kufanya michezo mbalimbali. Akijibu baadhi ya changamoto zilizoainishwa katika taarifa hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Mheshiwa Jamila Yusuph ameahidi kushughulikia upatikanaji na uandaaji wa viwanja vya michezo ambavyo vitakuwa tayari kabla ya mwisho wa mwezi wa tisa mwaka huu.
Meneja wa Benki ya CRDB kanda ya Nyanda za Juu Kusini Bi. Jenifer Tondi (kushoto) akiwa na wanafunzi pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Mheshiwa Jamila Yusuph (Kulia) wakati wa kukabidhi viti na meza 60.
Mpanda to Tabora road
Anuani ya Posta: P.O.Box 688 Mpanda
Simu : 025 295 5164
Simu: 025 295 5164
Barua pepe: ded@nsimbodc.go.tz
Hatimiliki@2016GWF.Haki zote zimehifadhiwa