Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo Mkoani Katavi imeendelea kutekeleza afua mbalimbali za lishe kwa kufuata Mwongozo wa Taifa wa Lishe, Mpango Jumuishi wa Taifa wa Pili (2021/2022-2025/2026), pamoja na sera mbalimbali za nchi zinazolenga kuzuia na kupambana na udumavu na utapiamlo mkali kwa watoto chini ya miezi 59.
Hayo yamebainishwa katika kikao kazi cha kamati ya Lishe Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo Mkoani Katavi kilichoketi leo katika ukumbi wa mikutano uliopo katika halmashauri hiyo, kilichoongozwa na Kaimu Mkurugenzi mtendaji ambaye pia ni afisa utumishi katika halmashuri hiyo Bi Magdalena Lugange.
Bi. Lugange amesema halmashauri hiyo imejipanga kutokomeza udumavu hasa kwa watoto kupitia mpango wa lishe bora mashuleni kupitia programu ya lishe bora katika kaya za wananchi pamoja na taasisi zilizopo katika halmashauri hiyo hasa mashuleni.
Katika kutekeleza adhma hiyo kikamilifu, Bi. Magdalena Lugange ameagiza wajumbe wa kamati ya lishe katika halmashauri hiyo kuandaa mpango madhubuti wa kuhamasisha lishe bora kwa kushirikiana na wadau mbalimbali hasa viongozi wa vijiji na kata, wazazi, mashirika na taasisi mbalimbali zinazotoa huduma katika halmashauri hiyo.
Kwa upande wake, mkuu wa idara ya Elimu Sekondari Mwalimu. Elisonguo Mshiu amesema shule zote 17 za sekondari katika halmashauri hiyo ya Nsimbo zinatoa huduma ya chakula kwa wanafunzi kwa kushirikisha wazazi na walezi pamoja na wadau wengine ili kuhakikisha watoto wanapata elimu bora na kwa wakati.
Pamoja na mafanikio yaliyopatikana kwa upande wa idara ya elimu sekondari kuhakikisha shule zote 17 zinatoa huduma ya chakula, mkuu wa idara ya elimu msingi Mwalimu Andrea Malyati asema angalau shule 64 kati ya 69 zinatoa huduma ya chakula katika maeneo yao. Aidha, mwalimu Malyati amesema bado jitihada zinaendelea kufanyika kwa kutoa elimu na hamasa kwa wazazi/walezi na wadau wengine ili kuhakikisha shule zote 69 katika halmashauri hiyo zinatoa huduma ya chakula ili kuwaweka wanafunzi katika hali ya utulivvu wawapo madarasani na kudhibi utoro unaosababishwa na ukosefu wa huduma ya chakula mashuleni.
Mganga mkuu wa Wilaya ya Nsimbo Dkt. Martin Mwandiki ameishukuru serikali kupitia uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo kwa kutoa kiasi cha shilingi milioni 26,572,132/= sawa na 129.63% ya fedha zilizoombwa yaani kiasi cha shilingi milioni 21,024,023/= fedha mabazo zimetumika kutekeleza programu hiyo ya lishe bora wilayani Nsimbo.
Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mkataba wa lishe ngazi ya Halmashauri kwa kipindi cha kuanzia mwezi Aprili hadi Juni katika mwaka wa fedha 2024/2025, afisa lishe katika Halmashauri hiyo Bi. Zakina Issa amesema wamejijapanga kutokomeza kabisa udumavu kwa watoto walioko chini ya miezi 59 kwa kutoa elimu kuhusiana na lishe bora kwa watoto mashuleni na vituo mbalimbali vinavyotumika katika makuzi ya watoto (daycare).
Bi. Zakina amesema Pamoja na mpango huo wa kutokomeza udumavu kwa watoto, Halmashauri hiyo pia inalenga kuzuia na kupambana na magonjwa yasiyoambukiza yatokanayo na mtindo wa maisha kama ulaji mbovu na magonjwa mengine kama vile saratani, kisukari na shinikizo la damu. Sambamba na hayo, amesema Halmashauri hiyo pia inatoa huduma mbalimbali zikiwemo matibabu ya utapiamlo mkali kwa watoto wenye umri wa miezi 6-59 kwa kutumia vyakula dawa vinavyotolewa katika vituo vya kutolea huduma, kutoa elimu ya lishe kwa wananchi kupitia Siku ya Afya na Lishe ya Kijiji (SALIKI).
Aidha, utoaji wa matone ya Vitamini A na dawa za kuua minyoo ya tumbo kwa watoto chini ya miaka mitano, utoaji wa vidonge vya kuongeza wekundu wa damu kwa wajawazito, na elimu ya unyonyeshaji na ulishaji unaofaa kwa wazazi/walezi wa watoto wenye umri wa chini ya miezi 23 imeendelea kutolewa kikamilifu katika vituo vya kutolea huduma za afya na kwenye jamii kupitia watoa huduma ngazi ya jamii (WAJA/CHW).
Katibu wa kamati ya Lishe ya Halmashauri ambaye pia ni Mkuu wa divisheni ya Afya, Huduma za Lishe na ustawi wa jamii
Wajumbe wa kamati ya Lishe wakifatilia wasilisho la utekelezaji wa afua za Lishe katika Halmashauri
Mpanda to Tabora road
Anuani ya Posta: P.O.Box 688 Mpanda
Simu : 025 295 5164
Simu: 025 295 5164
Barua pepe: ded@nsimbodc.go.tz
Hatimiliki@2016GWF.Haki zote zimehifadhiwa