Serikali ya awamu ya sita chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya maboresho makubwa ya huduma za kijamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo Mkoani Katavi kwa kuboresha na kujenga miundombinu mingi katika sekta mbalimbali.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo Bi. Christina Daniel Bunini amesema pamoja na idara zingine, idara ya Afya imeboreshwa katika kipindi cha uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo Halmashauri hiyo imefanikiwa kuongeza vituo vya kutolea huduma za afya hadi kufika 30 ambapo Hospitali ya Wilaya ni moja (1), Vituo vya Afya sita (06) kati ya hivyo, kituo kimoja kinamilikiwa na taasisi binafsi. Pamoja na vituo hivyo vya Afya, Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo pia ina Zahanati zipatazo ishirini na tatu (23) zinazohudumia wananchi
Hospitali ya Wilaya ya Nsimbo (Jengo la huduma za dharura)
Kituo cha Afya Itenk ni moja ya Vituo vya kutolea huduma ya Afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo
Kwa upande wa rasilimali watu, Bi Christina Bunini ameeleza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo ina jumla ya watumishi wa afya 312 sawa na asilimia 42 ya watumishi 742 wanaohitajika kuhudumia wananchi wapatao 201,102 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022. Pamoja na upungufu huo, wataalamu wa afya waliopo wamekuwa wakitekeleza ipasavyo majukumu yao ya kuwahudumia wananchi.
Katika kipindi cha uongozi wa Mheshimwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Idara ya afya imeendelea kuboreshwa kwa kiasi kikubwa kupitia vitengo vyake kama Utawala, Kitengo cha Afya ya Uzazi ya Baba, mama na mtoto, kitengo cha UKIMWI na kifua kikuu, kitengo cha Dawa, vifaa tiba na vitendanishi, kitengo cha huduma za maabara, kitengo cha chanjo na magonjwa yanayotolewa taarifa, kitengo cha Makusanyo ya Fedha na Bima, kitengo cha kudhibiti magonjwa yasiyopewa kipaumbele, kitengo cha kudhibiti Malaria, Magonjwa ya IMCI, kitengo cha afya na mazingira, kitengo cha ustawi wa jamii na kitengo cha huduma ya lishe. Vitengo vyote vimekuwa vikishirikiana katika majukumu mbalimbali jambo linalorahisisha utoaji wa huduma katika jamii kwa urahisi.
Aidha, kwa upande wa Divisheni ya Ustawi wa Jamii, makundi yote maalum ikiwemo wazee, Watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na watu wenye ulemavu yameendelea kuhudumiwa ipasavyo. Pamoja na hayo, Divisheni hii imeendelea pia kushughulikia huduma ya matunzo kwa makundi hayo ikiwemo usuluhishi wa migogoro ya ndoa.
Pamoja na majukumu hayo, idara ya Ustawi wa Jamii pia imeendelea kuratibu shughuli zote zinazofanywa na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayoshughulika na miradi ya UKIMWI, Lishe, Chanjo na Uhifadhi wa mazingira ili miradi yote ilete tija kwa wananchi Wilayani Nsimbo.
Hata hivyo, elimu ya lishe imeendelea kutolewa kwa makundi mbalimbali ya kijamii ikiwemo wajawazito na Watoto wenye umri chini ya miaka mitano, kugawa malighafi za kutengeneza vyakula dawa (F75 na F100) kwenye maeneo ambayo yana idadi kubwa ya watoto walioathirika na utapiamlo.
Hatua ya kujengwa kwa Zahanati na Vituo vya Afya zaidi katika Halmashauri hiyo kumewasaidia wananchi wengi kupata huduma karibu na makazi yao na kupunguza mwendo wa kutembea umbali mrefu wakifuata huduma za afya.
Katika kupunguza changamoto za usafiri kwa wagonjwa wa dharura katika jamii na kurahisisha huduma kwao, Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo imefanikiwa kupata Magari mawili ya kubebea wagonjwa (Ambulance), jambo linalorahisisha usafiri kwa wagonjwa na kuwafikisha katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa haraka
Gari la kubebea wagonjwa (Ambulance)
Mpanda to Tabora road
Anuani ya Posta: P.O.Box 688 Mpanda
Simu : 025 295 5164
Simu: 025 295 5164
Barua pepe: ded@nsimbodc.go.tz
Hatimiliki@2016GWF.Haki zote zimehifadhiwa