Pichani:Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Mh.Jamila Y.Kimaro akikabidhi mfano wa Hundi ya thamani ya Shilingi Mil. 122,500,000.00 kwa Wajasiriamali akina Mama Vijana na Wenye Ulemavu wakati wa Hafla ya kukabidhi mikopo hiyo Aprili 13,2021.katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Nsimbo.
Nsimbo-HQ
Zaidi ya Wajasiriamali 300 kutoka katika makundi ya kinamama Vijana na wenye ulemavu kutoka kata 12 za Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo wamenufaika na mkopo wa Shilingi 122,500,000 (Milioni Mia moja Ishirini na Mbili na Laki tano) ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali la kutenga asilimia 10 za mapato ya ndani kwa ajili ya kuwezesha Wajasiriamali Wanawake Vijana na Wenye Ulemavu kiuchumi kwa mwaka wa fedha 2020/2021.
Fedha hizo zimetolewa kwa vikundi 32 ambapo shilingi 57,000,000.00 zimetokana na Asilimia 10 ya mapato ya ndani na kiasi cha Shilingi 65,500,000.00 zimetokana na marejesho ya mikopo kutoka katika vikundi vilivyokopeshwa miaka iliyopita ambapo hadi kufikia Machi 2021 Halmashauri itakuwa imeshatoa jumla ya Tsh. 149,500,000.00 kwa vikundi 39 vya Wajasiriamali kati ya hivyo vya Wanawake ni vikundi 36 na Vijana ni vikundi 3.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi Hundi kwa Wajasiriamali wanufaika wa mkopo huo Aprili 13, 2021 Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Mh. Jamila Kimaro amewataka Wajasiriamali wa Nsimbo kutumia fedha hizo kwa malengo mahsusi ili kufikia azma ya Serikali kuwakwamua Wananchi waweze kuondokana na Umasikini.
Mh.Kimaro amebainisha kuwa sababu kubwa inayopelekea baadhi ya vikundi vya wajasiriamali Nchini kushindwa ni pamoja na kushindwa kutumia fedha kwa ajili ya malengo mahsusi jambo linalopelekea changamoto ya kutorejesha mikopo kwa Wakati.
Ameeleza kuwa ni muhimu kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii Nsimbo kushirikiana kwa karibu na Viongozi wa Kisiasa kusudi Elimu iweze kuwafikia watu wa makundi mbalimbali ikiwemo makundi maalumu ya Walemavu ambao kwa Nsimbo wameonyesha muitikio mdogo kushiriki katika fursa hii muhimu iliyotolewa na Serikali.
Aidha Mh.Kimaro ameupongeza Uongozi wa Halmashauri kwa usimamizi makini wa kuhakikisha kuwa fedha za Mikopo zinarejeshwa kwa wakati na hivyo kuwezesha makundi mengine kukopa hatua ambayo inatoa fursa kwa engine kunufaika na fursa hiyo.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi katika Hafla hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo Bw.Mohamed Ramadhani amewataka Wajasiriamali kuwekeza zaidi katika elimu na ujuzi wa biashara kabla ya kuchukua Mikopo.
Ameeleza kuwa fedha pekee haiwezi kuleta matunda yaliyokusudiwa ikiwa Elimu ya biashara kwa Wajasiriamali,haitotolewa na hivyo kuwataka Wajasiriamali hao kuwekeza zaidi katika kutafuta maarifa na Elimu ya Biashara ili waweze kupata faida
Amesema ni muhimu kwa Wajasiriamali kutanua wigo wa biashara kwa kuondokana na biashara za muda mfupi na badala yake walenge kuanzisha biashara za Uwekezaji ili waweze kujikwamua na umasikini.
Amesisitiza Wajasiriamali kuhakikisha kuwa mitaji inakua, kuzingatia muda wa marejesho sambamba na kutoa hamasa na elimu kwa wengine ili waweze kukopa kwa wingi ili kutoa fursa kwa wengi waweze kunufaika.
Mpanda to Tabora road
Anuani ya Posta: P.O.Box 688 Mpanda
Simu : 025 295 5164
Simu: 025 295 5164
Barua pepe: ded@nsimbodc.go.tz
Hatimiliki@2016GWF.Haki zote zimehifadhiwa