Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, Bi. Christina Bunini, amekabidhi mizinga kwa wanachama wa Chama cha Ushirika wa Mazao ya Nyuki kama sehemu ya juhudi za kuongeza uzalishaji na kuinua sekta ya ufugaji nyuki katika wilaya hiyo. Tukio hilo limefanyika wakati wa ziara ya kikazi ya Mradi wa BEVAC, unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya kupitia shirika la Enabel, kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Bi. Bunini amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya Serikali na wadau wa maendeleo ya kuimarisha miundombinu ya sekta ya nyuki, sambamba na kuwawezesha wanavikundi kwa vitendea kazi muhimu ili kuongeza tija na kipato.
Ziara hiyo iliyoongozwa na Mratibu wa Mradi wa BEVAC, Bi. Flosia Vugo, imelenga kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo cha kisasa cha usindikaji wa mazao ya nyuki pamoja na kujionea namna wanachama wanavyoongeza thamani ya mazao yao kwa kutumia mbinu bora na zenye tija.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama, Bw. Peter Kalula, alisema chama hicho kilianza mwaka 2022 kikiwa na wanachama 80 na hadi Julai 2025 wamefikia wanachama 170, ikiwa ni pamoja na wanawake 30. Alisema ongezeko hilo linaonesha hamasa kubwa kutoka kwa jamii na uwezo wa sekta ya nyuki kubadilisha maisha ya wananchi.
Hata hivyo, alitaja changamoto kama vile umbali wa ofisi za utoaji vibali, gharama kubwa za vibali, na ukosefu wa masoko ya uhakika kwa bidhaa zao. Alitoa wito kwa Serikali na Mradi wa BEVAC kusaidia upatikanaji wa mikopo na kufungua masoko ya kudumu.
Mwakilishi wa Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji, Bw. Kayumba Torokoko, aliwapongeza wanachama kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa kituo na akawahimiza kuanzisha vyanzo mbadala vya mapato ili kujiimarisha kiuchumi.
Mradi wa BEVAC umeendelea kuonyesha dhamira ya kuinua sekta ya ufugaji nyuki kwa kusaidia uboreshaji wa miundombinu, kutoa mafunzo ya kitaalamu, na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, wadau wa maendeleo, na jamii. Kwa msaada huu endelevu, ndoto za wananchi wa Nsimbo kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa mazao ya nyuki zinaendelea kutimia.
Mpanda to Tabora road
Anuani ya Posta: P.O.Box 688 Mpanda
Simu : 025 295 5164
Simu: 025 295 5164
Barua pepe: ded@nsimbodc.go.tz
Hatimiliki@2016GWF.Haki zote zimehifadhiwa