Kaimu Mkuu wa Idara ya Ujenzi Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo Mhandisi Martin Kasonso akitoa maelezo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Mh.Jamila Kimaro alipotembelea Kituo cha Afya Ugalla 14 Machi Machi 2022 kujionea maendeleo ya Ujenzi wa Mradi huo.
TAARIFA KWA UMMA
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo imesikitishwa na Habari za uongo zenye viashiria vya nia ovu zilizosambazwa kupitia makundi mbalimbali ya Watsup pamoja na Mitandao ya kijamii zilizochapishwa na Mwandishi wa Habari wa Blogu ya Katavi kwanza zikielezea madai ya kusimama kwa ujenzi wa Mradi wa Kituo cha Afya Ugalla kwa Muda wa Wiki mbili pamoja na madai ya Mkandarasi kutolipwa kwa muda wa wiki mbili.
Habari hizo zilichapishwa kupitia Blogu ya Katavi Kwanza katika chapisho lake la Tarehe 13 Machi 2022 zikimnukuu Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Katambike akisema Ujenzi wa kituo cha Afya Ugalla umesimama kwa takribani wiki mbili.
Katika chapisho jingine Mwandishi wa Blogu ya Katavi kwanza alichapisha habari katika Blogu yake hiyo ikimnukuu Mwenyekiti wa Kijiji cha Katambike akisema Mkandarasi anayejenga Mradi huo hajalipwa fedha zake kwa muda Mrefu jambo lililopelekea kusimama kwa mradi huo.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo inalaani vikali kitendo cha kusambaza Habari hizo zisizo na ukweli wowote zenye viashiria vya nia Ovu ya kuichafua Taswira ya Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo kilichofanywa na Mwandishi wa Habari wa Blogu ya Katavi kwanza kwa maslahi yake binafsi na kwamba inatoa onyo kali kwa Mwandishi huyo wa Habari.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo inaujulisha Umma wa Watanzania kuwa Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Afya Ugalla haukusimama kama ilivyoelezwa na Mwandishi wa Blogu ya Katavi kwanza na badala yake shughuli zote za Ujenzi zilikuwa zikiendelea kwa Takribani wiki mbili zilizopita hadi hatua ulipofikia mradi huo.
Ukweli ni kuwa katika Hoja ya kwanza Ujenzi wa Kituo cha Afya Ugalla mpaka hatua ulipofikia umetekelezwa kwa kipindi cha wiki tatu.Hadi kufikia 04 Machi 2022 na kwamba katika kipindi hicho shughuli mbalimbali za Ujenzi zilikuwa zikiendelea
Katika Hoja ya Pili ukweli ni kuwa Ucheleweshaji wa Malipo ya Mzabuni wa kusambaza mchanga,Mawe na Kokoto ulisababishwa na kamati ya Ujenzi ya Kituo hicho kutaka mzabuni alipwe fedha nyingi kuliko kiasi cha malighafi zilizofikishwa katika eneo la mradi jambo lililopelekea wataalam kujiridhisha na mzigo uliofika kabla ya kufanya malipo.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo inatoa wito kwa Waandishi wa Habari kote Nchini kuzingatia misingi ya taaluma yao ya Uandishi wa Habari ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa Habari zinatolewa kwa kuzingatia usawa ikiwa ni pamoja na kujiridhisha na pande zote mbili kabla ya kusambaza na kwamba haitosita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wale wote watakaosambaza Habari za Uongo dhidi ya Halmashauri.
Aidha Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji inawahakikishia Wanahabari kote Nchini kuwa itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa jambo lolote linalohitaji Ufafanuzi wa Kitaalamu kwa Waandishi wa Habari lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa Wananchi wanapata haki yao ya msingi ya Taarifa sahihi na kwa wakati pindi inapohitajika.
Imetolewa na;
John A.Mganga
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
HALMASHAURI YA WILAYA YA NSIMBO
Mpanda to Tabora road
Anuani ya Posta: P.O.Box 688 Mpanda
Simu : 025 295 5164
Simu: 025 295 5164
Barua pepe: ded@nsimbodc.go.tz
Hatimiliki@2016GWF.Haki zote zimehifadhiwa