Kampuni ya Premium Active (T) Limited, inayojihusisha na ununuzi wa tumbaku, imekabidhi madawati 201 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo kama sehemu ya mchango wake kwa jamii, hatua inayolenga kupunguza uhaba wa madawati mashuleni.
Makabidhiano hayo yamefanyika katika hafla iliyofanyika katika kijiji cha mwenge kilichopo katika kata ya Nsimbo, ikihudhuriwa na viongozi wa serikali na sekta binafsi. Mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Mhe. Jamila Yusuph Kimaro, ameipongeza kampuni hiyo kwa kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha elimu na kusaidia wanafunzi kupata mazingira bora ya kujifunzia.
Baada ya kupokea madawati hayo, Mhe. Kimaro alimkabidhi rasmi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Nsimbo, Bi. Christina Daniel Bunini, ambaye ameahidi kuyasambaza kwa shule zilizopo katika kata zenye uzalishaji wa zao la tumbaku ambazo alizitaja kuwa ni kata ya Katumba, Kanoge, na Ugalla. Miongoni mwa shule zitakazonufaika ni Bulembo, Kabuga, Kalungu, Kanoge, Kasisi, Lukama, Mtambo ambazo zitapewa idadi sawa ya madawati 25 huku Ivungwe ikipatiwa madawati 26.
Aidha ameagiza waalimu katika shule hizo kuyatunza madawati ikiwa ni pamoja na kuyafanyia ukarabati pale inapotakiwa.
Kwa mujibu wa Afisa Uzalishaji wa Premium Active Tanzania, Bw. Frank Ayoh, msaada huo ni sehemu ya utaratibu wa kampuni wa kurejesha asilimia 6 kwa kila kilo ya tumbaku inayouzwa. “Tuliwasiliana na idara ya elimu na kubaini kuwa mahitaji makubwa ni madawati, hivyo tumechangia shilingi milioni 14.7 kusaidia wanafunzi wa Nsimbo,” alisema.
Mkuu wa Kitengo cha Elimu Msingi, Bw. Frank Sichalwe, amesema madawati hayo yamechangia kupunguza uhaba uliokuwepo wa madawati 5,312. “Tunatoa wito kwa makampuni mengine kuiga mfano huu kwa kusaidia sekta ya elimu,” aliongeza.
Wanafunzi walionufaika na msaada huo wameeleza furaha yao, wakiahidi kuyatunza madawati kwa ajili ya vizazi vijavyo. Kasanga Ramadhani, aliyewakilisha wanafunzi, alisema: “Tutahakikisha tunawahamasisha wenzetu kuyatunza madawati haya kwa ustawi wa baadaye.”
Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na umma ili kuboresha mazingira ya elimu na kuhakikisha kila mwanafunzi anapata nafasi ya kusoma katika mazingira rafiki.
Mpanda to Tabora road
Anuani ya Posta: P.O.Box 688 Mpanda
Simu : 025 295 5164
Simu: 025 295 5164
Barua pepe: ded@nsimbodc.go.tz
Hatimiliki@2016GWF.Haki zote zimehifadhiwa