Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Mheshimiwa Jamila Yusuph amekabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi Milioni mia nne na ishirini (M420) pamoja na pikipiki kumi na moja (11) kwa wajasiriamali wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo Mkoani Katavi katika hafla ya utoaji wa mikopo ya asilimia kumi kutoka mapato ya ndani inayotolewa na halmashauri. Hafla iliyofanyika leo katika ukumbi wa shule ya sekondari Nsimbo Mkoani Katavi imehudhuriwa na vikundi hamsini na sita vya wajasiriamali walionufaika na mkopo huo.
Mheshimiwa Jamila Yusuph amewasihi wajasiriamali hao walionufaika na mikopo hiyo kutumia fedha hizo kwa miradi na malengo yaliyokusudiwa ili kuepuka changamoto wakati wa urejeshwaji. Katika hafla hiyo, takribani vikundi hamsini na sita vilivyosajiliwa ikijumuisha makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wamepokea kwa furaha mikopo hiyo inayolenga kuwainua kiuchumi.
Katika kuimarisha usimamizi na uendeshwaji wa miradi iliyokusudiwa na wajasiriamali hao, Mheshimiwa Jamila Yusuph amewakumbusha maafisa maendeleo ya jamii katika ngazi zote halmashauri ya wilaya ya Nsimbo kuendelea kuwatembelea wanufaika hao na kutoa elimu ili wayafikie matarajio yaliyopangwa wakati wa uombaji wa mikopo hiyo ili kusudi iwe na tija kiuchumi.
Mheshimiwa Jamila amewatia moyo waombaji waliokosa fursa ya mikopo hiyo kutokata tamaa kwani serikali bado inaendelea kutenga fedha kwaajili ya makundi lengwa kila mwaka, hivyo waendelee kujishughulisha wakati wakisubiri fursa hiyo wakati mwingine kwakuwa wombaji ni wengi na bajeti ni ndogo, jambo lililosababisha baadhi ya waombaji kukosa mikopo hiyo.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya ya Mapanda mheshimiwa Jamila Yusuph ametumia fursa hiyo kukemea vitendo vya ukatili vinavyotokea katika jamii hasa vikihusisha makundi ya watoto na wanawake. Amewakumbusha wazazi kuendelea kuwalinda watoto hasa kwa kukaa na kuwa karibu na watoto wao ili iwe rahisi kufahamu viashiria vya ukatili na changamoto zingine wanazopitia katika familia, jamii na hata mashuleni ili kuwasaidia mapema kabla hayajawathiri.
Aidha, Mheshimiwa Jamila amewakumbusha wananchi Wilayani Nsimbo kuzingatia lishe bora ili wawe na afya njema na imara na hivyo kutekeleza majukumu yao kwa wakati na kwa weledi mkubwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo Bi. Christina Bunini amewasihi wanufaika wa mikopo hiyo kufanya marejesho bila kufuatiliwa wala kusuasua ili iweze kuwanufaisha waombaji wengine kwa wakati kama ambavyo wao wamepata fursa hiyo.
Wakati huohuo Bi. Christina Bunini amewaasa wanufaika wa mikopo hiyo hasa kundi la maafisa usafirishaji (bodaboda) kuendesha pikpiki kwa tahadhari muda wote wakiwa katika hali ya utimamu wa mwili na akili ili kuepusha ajali zinazoepukika.
Kabla ya makabidhiano ya mfano wa hundi, akitoa taarifa ya mwenendo mzima wa mikopo hiyo, Mkuu wa idara ya Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo Bwana Rodrick Kidenya amesema jumla ya vikundi mia moja na nne (104) vilijitokeza kuomba mikopo hiyo ambapo viliomba jumla ya shilingi bilioni moja na milioni mia saba (Bilioni 1.7).
Bwana Kidenya amesema kulingana na ufinyu wa bajeti, ni vikundi hamsini na sita tu ndivyo vilivyopewa kipaumbele na kukabidhiwa mikopo hiyo ambapo wanapaswa kurejesha ndani ya mwaka mmoja.
Awali akitoa elimu kwa vikundi hivyo, Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Kanoge Wilayani Nsimbo Bi. Hollo Mbagga amekumbusha wajasiriamali hao namna bora ya kusimamia rasilimali, ikiwa ni pamoja na ushirikiano ulio bora, mawasiliano kwa wakati, ufuatiliaji na tathmini pamoja na kutochoka kujifunza ili kuboresha miradi yao waliyokusudia kuianzisha.
Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na Katibu tawala wa Wilaya ya Mpanda Bwana Juma Abdalla, wanufaika kutoka jumla ya vikundi hamsini na sita wamekabidhiwa mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi milioni mia nne na ishirini pamoja pikipiki kumi na moja kwaajili ya kundi la maafisa usafirishaji.
Mpanda to Tabora road
Anuani ya Posta: P.O.Box 688 Mpanda
Simu : 025 295 5164
Simu: 025 295 5164
Barua pepe: ded@nsimbodc.go.tz
Hatimiliki@2016GWF.Haki zote zimehifadhiwa