Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, ameongoza sherehe ya uzinduzi wa msimu wa ununuzi wa pamba na mazao mengine kwa mwaka 2025/2026, hafla iliyofanyika katika Kijiji cha Kapalala, Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo. Tukio hilo limehudhuriwa na viongozi wa serikali, vyama vya ushirika (AMCOS), wakulima, na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo.
Katika hotuba yake, Mhe. Mrindoko amewataka wakuu wa wilaya kusimamia kwa karibu uuzaji wa mazao kupitia vituo na mifumo rasmi ya serikali ili kudhibiti uuzaji holela unaosababisha hasara kwa wakulima pamoja na uhaba wa chakula majumbani.
Amesisitiza kuwa mazao ya pamba na tumbaku—yanayohusisha wakulima wengi mkoani humo—yanapaswa kuendeshwa chini ya usimamizi makini wa vyama vya msingi vya ushirika. Ameeleza kuwa baadhi ya viongozi wa vyama wamekuwa wakikiuka taratibu kwa kuingia mikataba isiyo rasmi na wakulima, jambo linalowaumiza wakulima kibiashara. Hivyo, amewaagiza wakuu wa wilaya kuhakikisha kilimo cha mkataba kinasimamiwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na miongozo ya serikali.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa ametangaza kuwa Katavi itaanza kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani, kuanzia na zao la ufuta katika msimu huu wa 2025/2026. Amehimiza wakulima kuunga mkono mfumo huo kwa kuwa unalenga kutoa bei nzuri, usalama wa soko, na kupunguza unyonyaji kutoka kwa walanguzi.
Aidha, ameipongeza kampuni ya NGS Investment Company Ltd kwa kuendelea kuwa soko la uhakika la zao la pamba mkoani humo. Amewataka wakulima kuhakikisha wanachuma pamba kwa usafi, kuipepeta vizuri na kuifikisha sokoni ikiwa katika ubora unaokubalika ili kukidhi mahitaji ya soko.
Akizungumza kwa niaba ya Bodi ya Pamba, Bw. Bugelaha Filbert amesema kuwa ili mkulima anufaike na kilimo cha pamba, ni lazima azalishe kwa tija—kwa kutumia mbegu bora, mbolea, na matunzo sahihi. Amesema kuwa mkulima anaweza kuvuna hadi kilo 1,000 kwa hekari moja ikiwa atazingatia kanuni hizo.
Kwa upande wao, wananchi waliohudhuria hafla hiyo wameeleza kufurahishwa na kuanza kwa msimu mpya wa ununuzi wa pamba, wakisema kuwa matumizi ya mizani bora na ya kisasa yameongeza matumaini ya kupata haki katika vipimo. Wameiomba serikali kuhakikisha kuwa malipo ya pamba yanafanyika kwa wakati ili kuwawezesha kujipanga kwa msimu mwingine wa kilimo na shughuli za kijamii.
Katika kauli yake ya mwisho, Mkuu wa Mkoa Mhe. Mrindoko amewahimiza vijana wa Katavi kutumia msimu huu kama fursa ya kuwekeza kwenye kilimo, akisisitiza kuwa ni sekta inayotoa ajira, kipato, na mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa.
Kapalala, Nsimbo – Juni 9, 2025
Mpanda to Tabora road
Anuani ya Posta: P.O.Box 688 Mpanda
Simu : 025 295 5164
Simu: 025 295 5164
Barua pepe: ded@nsimbodc.go.tz
Hatimiliki@2016GWF.Haki zote zimehifadhiwa