Mkoa wa Katavi umeandaa tamasha kubwa la Samia Day kwa lengo la kuadhimisha na kutangaza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Tamasha hilo linatarajiwa kufanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 4 hadi 5 Julai, 2025, katika Viwanja vya Shule ya Msingi Inyonga, Halmashauri ya Wilaya ya Mlele. Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mheshimiwa Mwanamvua Hoza Mrindoko.
Akizungumza na waandishi wa habari Julai 2, 2025, Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Bw. Albert Msovela, alisema kuwa lengo kuu la tamasha hilo ni kumpongeza na kumshukuru Rais Samia kwa mchango wake mkubwa wa kuleta maendeleo mkoani humo, ambapo zaidi ya shilingi trilioni 1.3 zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Kaulimbiu ya tamasha hili ni: ‘Asante Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Fedha za Maendeleo; Katavi Imara, Maendeleo Imara’. Tukio hili linahusisha Serikali ya Mkoa wa Katavi, taasisi mbalimbali na kundi maalum la burudani linalojulikana kama Mkasi Utaongea,” alisema Msovela.
Tarehe 4 Julai, 2025, timu ya Mkasi Utaongea, viongozi wa Serikali na wataalam mbalimbali watatembelea Hifadhi ya Taifa ya Katavi kujionea vivutio vya utalii na kufanya ziara kwenye miradi ya kimkakati ikiwemo Mradi wa Maji wa Miji 28 – Shanwe, vihenge vya kisasa vya kuhifadhia mazao, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na kituo cha kupozea umeme kutoka Grid ya Taifa.
Katika siku hiyo pia kutafanyika ‘Usiku wa Mama Samia’ katika Ukumbi wa Mpanda Social Hall, ambapo viongozi na wadau mbalimbali watapata fursa ya kujadili maendeleo ya Mkoa – tulikotoka, tulipo, na tunakoelekea.
Kilele cha Samia Day kitafanyika Julai 5, 2025, ambapo shughuli zitaanza na matembezi ya hiari kuanzia saa 1:30 asubuhi katika Mji wa Inyonga, yakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Mrindoko.
Michezo na burudani zitakazofanyika ni pamoja na mpira wa miguu, kuvuta kamba, kukimbia kwa magunia, kufukuza kuku na mbio za mita 100.
Msovela alitoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Katavi kujitokeza kwa wingi kushiriki kwenye tamasha hili la kihistoria, huku akihimiza ushiriki wa makundi yote ya jamii ikiwemo bodaboda, bajaji, mama lishe, machinga, wasanii na wananchi wote kwa ujumla.
Alizitaka pia taasisi za Serikali na zisizo za Serikali, mashirika ya kiraia, sekta binafsi na wadau wa maendeleo kushiriki kwa pamoja katika maadhimisho haya, kama ishara ya mshikamano na shukrani kwa mafanikio yaliyopatikana
Mpanda to Tabora road
Anuani ya Posta: P.O.Box 688 Mpanda
Simu : 025 295 5164
Simu: 025 295 5164
Barua pepe: ded@nsimbodc.go.tz
Hatimiliki@2016GWF.Haki zote zimehifadhiwa