Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, Bi. Christina Daniel Bunini, ametoa wito kwa ushirikiano wa dhati kutoka kwa viongozi wa kata, vijiji, idara mbalimbali pamoja na jamii kwa ujumla ili kufanikisha mapambano dhidi ya tatizo la udumavu.
Akizungumza wakati wa kufunga kikao cha Kamati ya Lishe kwa robo ya tatu ya mwaka kilichofanyika katika ukumbi mdogo wa Halmashauri, Bi. Christina Bunini amesema kuwa mafanikio katika vita dhidi ya udumavu yanahitaji juhudi za pamoja na mshikamano wa kijamii, hasa katika ngazi ya familia.
“Vita dhidi ya udumavu inahitaji kila mmoja wetu kushika ‘bunduki’ yake – iwe ni elimu, usimamizi, ushirikishwaji wa jamii au rasilimali – ili tufanikishe mapinduzi ya lishe,” alisisitiza Bi. Bunini mbele ya wajumbe wa kamati hiyo na wadau mbalimbali wa sekta ya lishe na afya.
Katika kikao hicho, wajumbe wamejadili kwa kina changamoto zinazosababisha udumavu pamoja na kutoa mapendekezo mahsusi ya kuboresha utekelezaji wa afua za lishe katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri.
Bunini pia ameagiza kuanzishwa kwa kampeni maalum ya kuwahamasisha wazazi kushiriki katika utoaji wa chakula shuleni, kufuatia taarifa kuwa ni asilimia 53 tu ya shule zinazotoa chakula kwa wanafunzi – hali inayochangiwa na mwitikio mdogo wa baadhi ya wazazi.
Kwa upande wake, Afisa Lishe wa Wilaya, Bw. Nikson Johanes, amesema kuwa mafanikio ya mkakati wa lishe hayawezi kufikiwa bila ushiriki wa jamii, akibainisha kuwa uelewa na ushirikiano wa karibu na wananchi ni nyenzo muhimu ya kuinua afya ya watoto.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji amemwagiza Mganga Mkuu wa Halmashauri, Dkt. Bonifasi Masaga (aliyekuwa akikaimu nafasi hiyo), kuhakikisha kuwa bajeti inatengwa mahsusi kwa ajili ya kuwawezesha watoa huduma ya afya ngazi ya jamii kuwafikia wananchi na kutoa elimu ya lishe kwa ufanisi zaidi.
Kikao hiki ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati mpana wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo katika kupambana na lishe duni na kuijenga jamii yenye afya bora, yenye uwezo wa kujifunza na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.
Mpanda to Tabora road
Anuani ya Posta: P.O.Box 688 Mpanda
Simu : 025 295 5164
Simu: 025 295 5164
Barua pepe: ded@nsimbodc.go.tz
Hatimiliki@2016GWF.Haki zote zimehifadhiwa