Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, Eng. Stephano B. Kaliwa, amewataka viongozi wa serikali za vijiji kuacha mila potofu na kufanya kazi kwa weledi ili kuhakikisha utekelezaji wa miradi na shughuli za maendeleo unafanyika kwa ufanisi na kwa mujibu wa sheria. Akizungumza katika mafunzo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Shule ya Sekondari Nsimbo kwa viongozi wa serikali za mitaa, yaliyojumuisha wajumbe wa serikali za Vijiji, wenyeviti wa Vitongoji, na maafisa watendaji wa Vijiji, Eng. Kaliwa alisisitiza umuhimu wa kuondokana na tamaduni zinazokwamisha maendeleo katika maeneo yao.
Mafunzo hayo yaliandaliwa na Chuo cha Serikali za Mitaa, Dodoma, yakilenga kuimarisha utawala bora na maendeleo endelevu katika ngazi za vijiji. Mafunzo hayo yalifunguliwa rasmi na Mkuu wa Chuo cha Serikali za Mitaa, ambaye alisisitiza umuhimu wa viongozi wa serikali za vijiji kuwa mstari wa mbele katika kuleta mabadiliko chanya kwa kufuata sheria na taratibu zilizopo.
Katika hotuba yake, Eng. Kaliwa ameonya dhidi ya vitendo vya kuua watu kwa tuhuma za uchawi, akisema kuwa tabia hizo hazikubaliki tena na zimepitwa na wakati. Amehimiza viongozi kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na taratibu ili kuleta maendeleo. Aidha, alibainisha kuwa viongozi wanapaswa kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha jamii inapata huduma bora.
Kuhusu suala la usimamizi wa mihuri ya serikali za vijiji, amefafanua kuwa mihuri inapaswa kuwa chini ya afisa mtendaji wa kijiji badala ya mwenyekiti wa kijiji. Amesema kuwa hatua hiyo inalenga kudhibiti matumizi yasiyo halali ya mihuri na kuboresha utendaji wa serikali za vijiji. Hata hivyo, mabadiliko hayo yaliibua maswali kutoka kwa baadhi ya viongozi waliokuwa na mashaka kuhusu ufanisi wa mfumo huo. Eng. Kaliwa aliwataka viongozi kufuata miongozo ya waraka wa utekelezaji na kuacha mjadala usio wa lazima.
Kwa upande wake, Mhadhiri Scholastica Nyabweke kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa, Dodoma, aliwahimiza viongozi wa serikali za vijiji kubuni vyanzo vipya vya mapato badala ya kutegemea tozo pekee. Alisema kuwa vyanzo hivyo vya mapato vitachangia kuongeza uchumi wa kijiji, vitongoji, na halmashauri kwa ujumla, huku akiwataka kuzingatia sheria, kanuni, na miongozo iliyotolewa na serikali.
Nyabweke ameleza kuwa changamoto kubwa inayowakabili viongozi wa vijiji ni ukosefu wa ufuatiliaji wa miradi na matumizi yasiyo ya uwazi ya rasilimali za umma. Alisema kuwa mafunzo hayo yataimarisha uwezo wa viongozi kusimamia rasilimali kwa uwazi na kushirikisha wananchi kikamilifu katika maendeleo.
Mmoja wa wawezeshaji wa mafunzo hayo amesema kuwa lengo kuu la serikali ni kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora kuanzia ngazi za chini. Aidha, amebainisha kuwa mafunzo haya yanaweza kupunguza migogoro ya ardhi na changamoto nyingine zinazowakabili viongozi wa ngazi za chini.
Mafunzo haya, yaliyoandaliwana Chuo cha mafunzo ya uongozi cha serikali za mitaa Dodoma kwa ajili ya kuimarisha utawala bora na maendeleo endelevu, yameacha matumaini makubwa kwa washiriki. Viongozi walihitimisha kwa kuahidi kuzingatia mafunzo hayo ili kuleta mabadiliko chanya katika maeneo yao na kuhakikisha rasilimali za kijiji zinasimamiwa kwa maslahi ya jamii nzima.
Mpanda to Tabora road
Anuani ya Posta: P.O.Box 688 Mpanda
Simu : 025 295 5164
Simu: 025 295 5164
Barua pepe: ded@nsimbodc.go.tz
Hatimiliki@2016GWF.Haki zote zimehifadhiwa