Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mheshimiwa Mwanamvua Hoza Mrindoko amewataka wataalamu kutoka Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo kuimarisha usimamizi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ili ikamilike kwa wakati.
Mheshimiwa Mrindoko ametoa wito huo Disemba 16, 2025 wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo Mkoani Katavi.
Katika mradi wa Ujenzi wa Ukumbi wa Mikutano unaoendelea katika makao makuu ya Halmashauri hiyo, Mheshimiwa Mrindoko amesema pamoja na changamoto zilizojitokeza mkandarasi lazima asimamiwe kwa ukaribu ili mradi huu unakamilika kwa wakati na kuanza kutumika.
“Hapa nitoe maelekezo kwamba ongezeni usimamizi, msimamieni vizuri mkandarasi mliyempatia mradi huu, kwa maana ya kuzingatia muda wa mkataba…….”
Mradi wa ujenzi wa ukumbi huo unatarajia kukamilika mwezi machi 2026 na hadi sasa ujenzi uko asilimia 20.
Mheshimiwa Mrindoko ametembelea pia mradi wa umaliziaji wa majengo katika Hospitali ya Wilaya ya Nsimbo ambapo amekagua umaliziaji wa jengo la utawala ambalo mradi huo umekamilika kwa asilimia 98 ambapo kazi iliyobaki ni marekebisho ya milango. Majengo mengine ni jengo la kufulia na jengo la bohari ya dawa ambayo yote yako katika hatua za mwisho kukamilika.
Aidha, katika jengo la upasuaji, Mheshimiwa Mrindoko amehimiza miundombinu iliyobaki ambayo ni mifumo ya umeme na maji kukamilika kwa haraka ndani ya siku kumi na nne ili huduma ya upasuaji ianze kutolewa katika Hospitali hiyo.
“fedha zimeshatolewa kwaajili ukamilishaji wa kila kipengele kinachohusiana na majengo haya na hasa jengo la upasuaji, ambalo nalo tumelikagua na tumeliona, sasa kwakuwa hii ndiyo kipaumbele na ndiyo malalamiko yaliyopo, mkurugenzi nikuagize, katika siku kimu na nne zinazokuja kuanzia leo hakikisha huduma za upasuaji zimeanza kutolewa kwenye hospitali hii….” Ameagiza RC Mrindoko.
Katika mradi wa ujenzi wa bwalo katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Katavi, Mheshimiwa Mwanamvua Mrindoko amewataka wakandarasi na wataalamu kutoka ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa asilimia mia moja ifikapo januari 31, 2026.
Wakati huo huo, mheshimiwa Mrindoko ametumia wasaa huo kuwahimiza wananchi kuwaandikisha watoto wanaotarajia kuanza elimu ya awali na msingi ili ifikapo Januari 13, 2026 watoto wote wenye sifa wanaanza shule. Sambamba na hilo, mheshimiwa Mrindoko amewahimiza wazazi wote ambao watoto wao wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza Januari 2026 kuhakikisha wanawapa mahitaji muhimu mapema ili kuepusha uchelewaji katika masomo yao.
Mheshimiwa Mrindoko ameendelea na ziara yake ambapo alipata wasaa wa kutembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa daraja la upinde wa mawe katika Kijiji cha Ikondamoyo ambapo mradi huo umekamilika kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Mrindoko amewasihi wananchi kulitunza daraja hilo na miundombinu ya barabara kwa ujumla ili liweze kudumu muda mrefu.
“Niwaombe sasa, hamasa ya wananchi wote kulitunza daraja hili na kutunza barabara hii iweze kudumu muda mrefu… mtunze miundombinu, maswala ya kuja kujaribu kubomoa kutafuta nondo zimepita wapi ili watu waibe, kulima karibu na barabara vyote hivyo vitaharibu miundombinu hii…” ameongeza Mheshimiwa Mrindoko
Kukamilika kwa mradi huo kumerahisisha mawasiliano kati ya wananchi wa kata ya Uruwira hususani wakazi wa Kijiji cha Ikondamoyo na vitongoji vyake waliokuwa wakipata changamoto za safari hasa wakati wa masika.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Mwanamvua Mrindoko amewasihi wananchi Mkoani Katavi kulima mazao yanayokomaa kwa muda mfupi kutokana na utabiri wa hali ya hewa kuonesha upungufu wa mvua katika msimu huu wa kilimo wa 2025/2026. Aidha, kutokana na uhaba huo wa mvua, Mheshimiwa Mrindoko amewasihi wananchi kutunza vyakula vilivyopo ili kuwa na uhakika wa chakula hadi msimu mwingine.
“Lakini linguine kubwa Zaidi, sasa hivi kila mmoja atunze chakula alicho nacho kuhakikisha kwamba kinaweza kutumika hata mpaka msimu mwingine unaokuja…..” ameongeza RC Mrindoko
Akizungumza mara baada ya ziara hiyo ya mkuu wa Mkoa, Diwani wa Kata ya Uruwira Mheshimiwa Fotunata Shulla, amesema kukamilika kwa daraja hilo kumekuwa faraja kwa wakazi wa Kata hiyo hususani Ikondamoyo na Vitongoji vyake.
Nao baadhi ya wanakijiji cha Ikondamoyo wameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa usikivu na kuwasaidia kujenga daraja katika eneo hilo.
Mpanda to Tabora road
Anuani ya Posta: P.O.Box 688 Mpanda
Simu : 025 295 5164
Simu: 025 295 5164
Barua pepe: ded@nsimbodc.go.tz
Hatimiliki@2016GWF.Haki zote zimehifadhiwa