Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, mkoani Katavi, limefanya kikao chake cha pili katika ukumbi mdogo wa Halmashauri hiyo, ambapo wajumbe walijadili ajenda mbalimbali zilizowasilishwa na kamati za kudumu za Baraza hilo.
Kikao hicho kiliongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, Mheshimiwa Athumani Juma Fimbo, kwa kushirikiana na Katibu wa Baraza ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, Bi. Christina Bunini. Kikao hicho kilifanyika kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.
Katika kikao hicho, kamati mbalimbali za kudumu ziliwasilisha taarifa zao za kiutendaji kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba, 2025. Kamati hizo ni pamoja na Kamati ya Kudhibiti Ukimwi, Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira, Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango, Kamati ya Maadili, pamoja na Kamati ya Elimu, Afya na Maji.
Akijibu hoja kutoka kwa wajumbe wa Kamati ya Elimu, Afya na Maji, Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, Bw. Elisenguo Mshiru, alieleza kuwa wanafunzi wa kidato cha kwanza bado wanaendelea kuripoti shuleni. Aliongeza kuwa zoezi la uhamasishaji linaendelea kwa kuwahimiza wazazi na walezi wa watoto waliopata nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza kuhakikisha wanaripoti mapema ili kuanza masomo mara moja.
Aidha, Baraza hilo liliaridhia uthibitisho wa watumishi wawili waliokuwa wakikaimu katika nafasi zao, na kuthibitishwa rasmi kuwa wakuu wa idara. Watumishi hao ni Bi. Bertha Ng’eve, aliyethibitishwa kuwa Mkuu wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, pamoja na Bw. Petro Mwita aliyethibitishwa kuwa Mkuu wa Idara ya Miundombinu na Maendeleo ya Vijijini na Mijini.
Miongoni mwa wageni waalikwa waliohudhuria kikao hicho ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mpanda, Ndugu Joseph Anniseth Lwamba, Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Mheshimiwa Jamila Yusuph Kimaro, Katibu Tawala wa Wilaya ya Mpanda, Ndugu Juma A. Njeru, pamoja na wageni wengine kutoka Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Mpanda.

Mpanda to Tabora road
Anuani ya Posta: P.O.Box 688 Mpanda
Simu : 025 295 5164
Simu: 025 295 5164
Barua pepe: ded@nsimbodc.go.tz
Hatimiliki@2016GWF.Haki zote zimehifadhiwa