Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Mheshimiwa Jamila Yusuph, amewataka viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo mkoani Katavi kuhakikisha wanawawezesha vijana kwa kuwapatia mikopo itakayowasaidia kujikwamua kiuchumi.
Mheshimiwa Jamila ameyasema hayo Januari 22, 2026, alipokuwa akizungumza katika Kikao cha Pili cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi mdogo wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo. Ambapo amewataka Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo Mheshimiwa Juma Fimbo, pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bi Christina D. Bunini kuhakikisha kuwa makundi ya vijana na wanawake yanapewa kipaumbele katika utoaji wa mikopo ya asilimia kumi inayotolewa ndani ya halmashauri hiyo.
“Wapo vijana ambao tayari wana miradi inayoendelea, lakini wameomba kuwezeshwa zaidi ili kukuza shughuli zao na hatimaye kuweza kuwaajiri vijana wenzao. Imani yangu ni kwamba maombi hayo yatafanyiwa kazi na watapewa kipaumbele katika kupatiwa mikopo hiyo” alisema Mheshimiwa Jamila.
Aidha, Mheshimiwa Jamila amewataka viongozi wa halmashauri hiyo kuhakikisha kuwa utoaji wa mikopo unaambatana na elimu ya ujasiriamali, ikiwemo namna ya kutambua fursa za kiuchumi zilizopo ndani ya halmashauri hiyo na mbinu bora za uendeshaji wa biashara ili kuhakikisha kuwa wanapata faida katika miradi yao na kurejesha mikopo kwa wakati.
Kwa upande mwingine, Mheshimiwa Jamila ameiagiza Kamati ya Fedha ya Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo kufanya ufuatiliaji na ukaguzi wa mara kwa mara kwa vikundi vilivyonufaika na mikopo hiyo, kwa lengo la kutathmini maendeleo ya miradi yao na kuwasaidia kutatua changamoto wanazokumbana nazo, ili kufikia lengo kuu la mikopo hiyo ambalo ni kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi na kukuza maendeleo ya halmashauri pamoja na Taifa kwa ujumla.
Mpanda to Tabora road
Anuani ya Posta: P.O.Box 688 Mpanda
Simu : 025 295 5164
Simu: 025 295 5164
Barua pepe: ded@nsimbodc.go.tz
Hatimiliki@2016GWF.Haki zote zimehifadhiwa