Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Bw. Albert Msovela, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo kwa utekelezaji madhubuti wa maagizo ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), ikiwa ni sehemu ya majibu ya hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2023/2024
Pongezi hizo zilitolewa leo katika Baraza la Hoja la Halmashauri ya Nsimbo lililofanyika katika Ukumbi Mdogo wa Halmashauri, ambapo Bw. Msovela alihudhuria kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi.
Katika hotuba yake, Katibu Tawala alieleza kuwa madiwani wa Halmashauri ya Nsimbo wamekuwa sehemu muhimu ya mafanikio kutokana na ushirikiano wao wa karibu na wataalamu wa Halmashauri katika kutekeleza maagizo ya LAAC pamoja na kusimamia miradi ya maendeleo kwa ufanisi. Aidha, alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Bi. Christina Daniel Bunini, kwa uongozi wake wa kijasiri na kitaalamu. Alisema kuwa nidhamu ya kiutendaji inayojengwa kupitia usikivu wake ni msingi imara wa mafanikio ya Halmashauri hiyo.
Akizungumza mbele ya wajumbe wa Baraza la Madiwani, Bw. Msovela alisema kuwa Halmashauri ya Nsimbo imekuwa mfano wa kuigwa kwa kujibu na kutekeleza maagizo kwa weledi na kwa wakati, hatua inayoonesha uwajibikaji na uzingatiaji wa misingi ya utawala bora. “Pamoja na kuwepo kwa hoja, hatua zilizochukuliwa zinaonyesha dhamira ya dhati ya Halmashauri hii kuleta mabadiliko. Kama majibu yangewasilishwa kwa wakati na kwa vielelezo kamili, hoja nyingi zingeweza kuepukwa,” alisema.
Aliwataka watumishi waendelee kuzingatia sheria, taratibu na miongozo ya kazi ili kuhakikisha hoja zote zilizobaki zinapatiwa majibu sahihi kwa wakati.
Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa na Mkaguzi wa Ndani, Bw. Chambi Ngelela, Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo imepokea hati ya kuridhisha (Unqualified Opinion) kutoka kwa CAG. Ripoti hiyo imeonesha kuwa hoja 19 kati ya zilizowasilishwa zimefungwa, huku hoja 40 bado hazijafungwa, huku maagizo yote 6 ya LAAC yakiwa yametekelezwa.
Akihitimisha kikao hicho, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, Mhe. Halawa Charles Malendeja, kwaniaba ya Madiwani wote, alieleza kuwa mafanikio haya yametokana na mshikamano wa kweli kati ya wataalamu wa Halmashauri na viongozi wa kisiasa. Ushirikiano huo umewezesha utekelezaji mzuri wa mipango ya maendeleo na majukumu ya kiutawala kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Mpanda to Tabora road
Anuani ya Posta: P.O.Box 688 Mpanda
Simu : 025 295 5164
Simu: 025 295 5164
Barua pepe: ded@nsimbodc.go.tz
Hatimiliki@2016GWF.Haki zote zimehifadhiwa