Kamishna wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bi. Asina Omari, Atembelea mafunzo ya Waandikishaji Wasaidizi na Waendesha Vifaa vya Kielektroniki vya Bayometriki (BVR Kits) katika Jimbo la Nsimbo, ambapo alisisitiza umuhimu wa uadilifu, weledi, na uzingatiaji wa sheria katika utekelezaji wa majukumu ya uandikishaji wa wapiga kura kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Akizungumza katika mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Nsimbo, Kamishna Asina alisema kuwa mabadiliko yoyote yanayofanyika katika mfumo wa uandikishaji yanahitaji umakini mkubwa. Alieleza kuwa kila hatua ya mchakato huo inapaswa kutekelezwa kwa usahihi na uaminifu ili kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake ya kikatiba ya kupiga kura bila vikwazo vya kiutendaji.
“Elimu mliyoipata ni dira itakayowaongoza kutekeleza kazi zenu kwa vitendo. Hakikisheni mnafuata mwongozo wa Tume kwa umakini na kutimiza majukumu kwa uadilifu,” alisema Kamishna huyo.
Amesisitiza kuwa washiriki wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa ushirikiano, kwa kuzingatia sheria, taratibu na viapo vya uaminifu walivyoweka mbele ya Tume, kama ishara ya dhamira ya kufanya kazi kwa uwazi na ufanisi. Aliongeza kuwa ubora wa kazi yao ndio msingi wa kuaminika kwa mchakato mzima wa uchaguzi.
Kwa upande wake, Afisa Mwandikishaji wa Jimbo la Nsimbo, Bw. Adolf Issaya Semindu, alisema kuwa washiriki wamepewa maarifa ya matumizi sahihi ya vifaa vya uandikishaji, ujazaji wa fomu rasmi, utunzaji wa vifaa kama mashine za BVR, daftari la wapiga kura, na kudumisha usiri wa taarifa hadi pale taratibu rasmi zitakapokamilika.
“Watendaji hawa sasa wana uelewa wa nadharia na vitendo kuhusu zoezi la uandikishaji. Ni wajibu wao kuhakikisha wanatekeleza majukumu kwa weledi kwa mujibu wa sheria, kanuni na miongozo ya Tume,” alisema Bw. Semindu.
Mafunzo hayo yamehitimishwa kwa viapo vya uaminifu kutoka kwa Waandikishaji Wasaidizi, waliokiri kwa dhati kuwa watatekeleza majukumu yao kwa uwajibikaji na uadilifu wa hali ya juu. Washiriki pia walipata fursa ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi wa kina ili kuondoa mkanganyiko kabla ya kuanza kwa zoezi lenyewe.
Mafunzo haya ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kuhakikisha kuwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 unaendeshwa kwa uwazi, usalama na haki kwa wananchi wote.
Mpanda to Tabora road
Anuani ya Posta: P.O.Box 688 Mpanda
Simu : 025 295 5164
Simu: 025 295 5164
Barua pepe: ded@nsimbodc.go.tz
Hatimiliki@2016GWF.Haki zote zimehifadhiwa