Mkuu wa mkoa wa Katavi Mh. Mwanamvua Hoza Mrindoko amesisitiza umuhimu wa kuwapa wafanyabiashara wadogo nafasi na kuhakikisha kwamba wanapewa mabanda katika eneo la maonyesho ili waweze kuonyesha na kujitangaza katika biashara ama shughuli za kiuchumi wanazofanya. Alisema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonyesha jitihada zake za kuleta maendeleo ambayo yameonekana kusaidia sekta mbalimbali, ikiwemo biashara na ujasiriamali. Alisema hayo wakati akifungua rasmi maonyesho ya wiki ya mwanakatavi yanayoendelea kufanyika katika uwanja wa Azimio Manispaa Mpanda hadi ifikapo tarehe 31/10/2024 ambapo ni kilele cha maonyesho haya.
Katika hotuba yake, Mkuu wa Mkoa amesema kuwa wiki ya Mwanakatavi inafanyika kwa mafanikio makubwa, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kukuza uchumi na kutoa fursa kwa wafanyabiashara wakubwa na wadogo kuonyesha bidhaa na huduma zao. Alieleza kuwa haya ni maonyesho yaliyobeba matukio mengi yenye manufaa makubwa na yanayolenga kuitangaza Tanzania kwa ujumla. Amesema huduma sasa zimesogezwa karibu hivyo wananchi wajitokeze ili kupata huduma.
Aidha, amesema kuwa Maonyesho hayo yaliyoandaliwa kwa umakini yamewezesha wadau kuweka mabanda mbalimbali ambapo biashara na shughuli zote zimewekwa wazi kwa wananchi na wageni waliofika kwa wingi. Halmashauri zote za mkoa wa Katavi zilikuwa banda kwa ajili ya kuonyesha shughuli zake.
Vivyohivyo, Mkuu wa Mkoa alipata wasaa wa kutembelea mabanda mbalimbali likiwemo banda la Halmashauri ya Nsimbo ambalo lilikuwa limesheheni shughuli mbalimbali za kiuchumi na bidhaa nyingi za kilimo pamoja na lishe bora. Mkuu wa mkoa alifurahishwa na kuwepo kwa banda maalumu la kusikiliza kero za wananchi. Aliwataka wananchi kujitokeza ili kuwasilisha kero zao kwani Serikali ya Mama Samia ni sikivu na wote watahudumiwa kwa karibu.
Akiendelea kuhutubia katika ufunguzi wa maonyesho hayo, alitoa agizo kuwa mwaka ujao maonyesho ya wiki ya Mwanakatavi yanapaswa kufikia kiwango cha kimataifa. Lengo likiwa ni kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara kutoka mataifa mbalimbali. Alieleza kuwa Mkoa wa Katavi ni moja kati ya mikoa yenye vivutio vingi vya kuwavutia wageni hivyo itakuwa ni fursa ya kupata ongezeko la kiuchumi.
Katika ufunguzi wa maonyesho haya viongozi wa Serikali na Chama walihudhuria ambapo Mkuu wa Wilaya na viongozi wengine walitoa hotuba zenye kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika maonyesho haya na kukuza ushirikiano kati ya sekta za umma na binafsi.
Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Mh. Jamila Yusuph Kimaro aliwahimiza wafanyabiashara kuona umuhimu wa maonyesho haya kwani yanatoa fursa nyingi za kiuchumi. Alieleza kuwa kwa kuwa wafanyabiashara ni wengi ni vyema wanakatavi kujifunza ubunifu mpya kwa wengine ili kwa pamoja waweze kukua huku wakitangaza katavi kama sehemu ya utalii kwani kuna vivutio vingi ambavyo katika maonyesho hayo,
Kiongozi wa Chama pia alitoa nasaha zake akiwahimiza wananchi na wafanyabiashara kuendelea kutumia maonyesho haya kama jukwaa la kujitangaza na kuchangia ukuaji wa uchumi wa mkoa wa Katavi na Tanzania kwa ujumla.
Akihitimisha hotuba yake, Mkuu wa Mkoa alitoa rai kwa wananchi waliojiandikisha katika daftari la mkazi kuhakikisha wanajitokeza siku ya kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa tarehe 27/11/2024. Aliwakumbusha juu ya maendeleo yaliyofanywa na Serikali ya awamu ya sita. Alisema ni vyema kuchagua kiongozi bora atakayeendeleza mafanikio yaliyopo kwa kuwa ni maendeleo endelevu kama kauli mbiu ya wiki ya mwanakatavi inayosema ’’Katavi yetu,Chagua Viongozi Bora wa Serikali za Mitaa, Imarisha Uchumi kwa Maendeleo Endelevu’’
Mpanda to Tabora road
Anuani ya Posta: P.O.Box 688 Mpanda
Simu : 025 295 5164
Simu: 025 295 5164
Barua pepe: ded@nsimbodc.go.tz
Hatimiliki@2016GWF.Haki zote zimehifadhiwa