Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo tarehe 9 julai 2025 imeendesha mafunzo maalum kwa Watendaji wa Kata na Vijiji, yakilenga kuwajengea uwezo kuhusu mfumo wa anwani za makazi na umuhimu wa postikodi (Post Code) katika kuwahudumia wananchi, hususan waombaji wa mikopo ya serikali na taasisi za kifedha.
Mafunzo hayo yamefanyika kwa lengo la kuhakikisha watendaji hao wanakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu mchakato wa utambuzi wa makazi ya wananchi kupitia anwani rasmi, jambo ambalo limekuwa kikwazo kwa baadhi ya wananchi kupata huduma muhimu kutokana na kukosekana kwa uelewa wa matumizi sahihi ya anwani za makazi katika kutoa na kupokea huduma.
Awali wakati akizungumza na washiriki mgeni rasmi Bi Christina Daniel Bunini Mkurugenzi wa Halmashauri amesisitiza umuhimu wa kila mtendaji kuwa kusikiliza kwa umakini na kutekeleza kwa vitendo yale wanayojifunza ili kusaidia wananchi pindi wanapofika ofisini kupata huduma.
“Sitaki kusikia mwananchi anakosa huduma kwa sababu tu mtendaji hakuwepo au hajui kuhusu mfumo huu wa anwani za makazi. Kila mmoja atimize wajibu wake kikamilifu katika eneo lake la kazi,” alionya Mkurugenzi.
Aidha, amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuendelea kuwa sehemu ya maboresho ya mifumo ya utawala na utoaji huduma kwa wananchi, hasa kwa kuhakikisha wananchi wote wanakuwa na anwani rasmi za makazi.
Watoa mada katika mafunzo hayo walikuwa ni Katibu wa Kamati ya Wataalam ya uratibu wa Anwani za makazi na Postkodi na Afisa TEHAMA wa Halmashauri. Mada zilizotolewa zimegusa maeneo ya kisheria, kiutendaji na kiteknolojia kuhusu usimamizi wa anwani za makazi, matumizi ya mifumo ya kielektroniki, na jukumu la kila mtendaji katika kuhakikisha taarifa za maeneo yao zinatambuliwa rasmi.
Mpanda to Tabora road
Anuani ya Posta: P.O.Box 688 Mpanda
Simu : 025 295 5164
Simu: 025 295 5164
Barua pepe: ded@nsimbodc.go.tz
Hatimiliki@2016GWF.Haki zote zimehifadhiwa