Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo imeanza rasmi zoezi la kuhakiki na kutoa vitambulisho vya bima ya afya kwa wananchi wa vijiji mbalimbali ndani ya halmashauri hiyo huku zoezi hilo likilenga zaidi kaya zisizo na uwezo zilizo kwenye daftari la Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Zoezi hilo limeanza rasmi Februari 6, 2026, likiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Bima ya Afya kwa wote, huku matarajio yakiwa ni kuandikisha takribani wananchi 5,000 ifikapo mwisho wa zoezi hilo, na kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata huduma bora za matibabu bila kujali hali yake ya kiuchumi
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, Mratibu wa TASAF wilayani humo, Bw. Frankson Kalugendo, ambaye pia ni kiongozi wa zoezi hilo, amesema kuwa zoezi hilo linafanyika kwa ushirikiano kati ya TASAF na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Bw. Kalugendo ameongeza kuwa kaya maskini zinazofaidika na Mpango wa TASAF zinatarajiwa kuwa wanufaika wa kwanza wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ulioasisiwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande wake, Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Mkoa wa Katavi, Bw. Ally Mwakababu, amesema kuwa zoezi hilo linahusisha uhakiki wa majina ya wananchi waliopo kwenye mpango wa TASAF, na ugawaji wa kadi za bima ya afya kwa wote watakao thibitishwa, ili waanze kunufaika na huduma za matibabu bure kupitia Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote.
Aidha, Bw. Mwakababu ameushukuru uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo kwa maandalizi mazuri, hususan katika kuhamasisha na kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kujiandikisha katika Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, pamoja na kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa amani na ufanisi.
Akizungumza mara baada ya kupatiwa kadi yake ya bima ya afya, mmoja wa wanufaika kutoka Kata ya Mtapenda, Bw. Deus Eusabius, amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwakumbuka wananchi wenye uhitaji na kubainisha kuwa mpango huo utasaidia kuokoa maisha ya wengi waliokuwa wakishindwa kupata matibabu kutokana na ukosefu wa fedha.
Zoezi hilo linatarajiwa kufanyika katika kata zote za Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo. Ambapo kwa sasa, limeanza katika Kata za Kapalala, Mtapenda, Nsimbo na Uruwila, likihusisha vijiji vyote vilivyopo ndani ya kata hizo, kabla ya kuendelea katika kata nyingine ili kuhakikisha kuwa wananchi wote wenye sifa wananufaika na mpango huo

Mpanda to Tabora road
Anuani ya Posta: P.O.Box 688 Mpanda
Simu : 025 295 5164
Simu: 025 295 5164
Barua pepe: ded@nsimbodc.go.tz
Hatimiliki@2016GWF.Haki zote zimehifadhiwa