Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mheshimwa Mwanamvua Hoza Mrindoko amewasihi mawakala na wafanyabiashara wa pembejeo za kilimo kuuza kwa bei elekezi na kujiepusha kupandisha bei kinyemela.
Mheshimiwa Mrindoko ameyasema hayo leo wakati akizindua msimu wa Kilimo kwa mwaka 2025/2026 uliofanyika katika viwanja vya ukumbi wa Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi. Mheshimiwa Mrindoko amewaagiza wakuu wa Wilaya katika Mkoa huo kusimamia vizuri uuzaji wa pembejeo za kilimo hasa mbegu na mbolea za ruzuku zinazotolewa na serikali.
Kuelekea msimu wa kilimo kwa mwaka 2025/2026, wadau mbalimbali wa kilimo, mifugo pamoja na wananchi kwa ujumla wamejumuika pamoja katika maonesho ya kilimo na mifugo yaliyofanyika kwa siku mbili katika viwanja vya ukumbi wa Mikutano uliopo katika Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi.
Akizungumza katika uzinduzi wa msimu wa kilimo uliofanyika Novemba 19 mwaka huu, Mgeni rasmi ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mheshimiwa Mwanamvua Hoza Mrindoko amewashukuru wadau wa kilimo Mkoani humo kujitokeza kufanya maonesho hayo kwa weledi na kuwataka kuendeleza ari hiyo katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mheshimiwa Mrindoko amesema maonesho hayo yaliyofanyika yawanufaishe wananchi wote walioshiriki na hata walioshindwa kushiriki ili yalete tija kwao na jamii kwa ujumla. Amewasihi wakulima kuendelea kutumia zana bora na za kisasa pamoja na pembejeo bora katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara huku wakiendelea kutumia elimu wanayopewa na maafisa ugani katika maeneo yao.
Aidha, Mheshimiwa Mrindoko Amewaagiza watendaji wote katika mkoa huo kuwafuata wakulima mashambani na kuwapa elimu ya namna bora ya kuzalisha kwa tija katika shughuli wanazozifanya. Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wakuu wa wilaya, wakurugenzi, makatibu tawala, makatibu kata, maafisa ugani, katika Mkoa wa Katavi kusimamia Upatikanaji wa mbolea na mbegu bora.
“wakuu wa wilaya simamieni vizuri ili mbolea na mbegu ziuzwe kwa bei ya ruzuku, hakikisheni hakuna wakala au wafanyabiashara watakaouza kwa bei tofauti”
Mheshimiwa Mrindoko amesema Matumizi sahihi ya mbegu na mbolea isimamiwe vizuri ili kuleta tija kwa wakulima ili kuepeusha malalamiko yatakayoweza kutokea iwapo wakulima watakosea kutumia kwa usahihi.
“Hakikisheni mnawaongoza na kuwaelimisha wakulima juu ya Matumizi sahihi ya zana bora na za kisasa za kilimo, matumizi ya matrekta makubwa na madogo, mashine za kupandia na kuvunia, mbegu bora na aina ya mbolea kulingana na mashamba ya wakulima …”
Amewataka Maafisa ugani kutekeleza majukumu waliyoajiriwa nayo kwa weledi na kuepuka kukaa maofisini kwa muda mrefu, ili kuwa karibu na wakulima na hatimaye waweze kuzalisha kwa tija.
“Hakikisheni mko katika kazi mlizoajiriwa nayo, ambayo ni kuwatumikia wakulima na wafugaji na kuwapa maelekezo na mfano bora ili kupata tija tunayoihitaji” ameongeza Rc Mrindoko
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amewapongeza wataalamu wote wa masoko kusimamia vizuri mfumo wa stakabadhi ghalani kwani umeanza kufanya kazi kwa tija kubwa katika mkoa wa katavi katika msimu wa kilimo uliopita Mheshimiwa Mrindoko amesema mazao yaliyouzwa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani kwa mwaka huu yamewanufaisha wakulima ambapo kiasi cha Shilingi 11,648,657,250 zimelipwa kwa wakulima na wafanyabiashara wa mazao ya kilimo mkoani katavi katika msimu wa kilimo wa mwaka 2024/2025.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mheshimwa Mwanamvua Mrindoko amesema Serikali ya awamu ya sita itaendelea kusimamia wakumila na wafanyabiashara kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani ambao unaleta tija kwa wakulima na si wengine.
Katika uzinduzi wa msimu wa kilimo mwaka huu, maonesho mbalimbali yamefanyika kutoka halmashauri zote za Mkoa wa Katavi pamoja taasisi mbalimbali hasa zinazojihusisha na masuala ya kilimo na mifugo.


Mpanda to Tabora road
Anuani ya Posta: P.O.Box 688 Mpanda
Simu : 025 295 5164
Simu: 025 295 5164
Barua pepe: ded@nsimbodc.go.tz
Hatimiliki@2016GWF.Haki zote zimehifadhiwa