Wakulima katika Halmashauri ya Wilaya Nsimbo wametakiwa kulima kwa kufuata njia za kisasa ikiwa ni pamoja na kuzingatia maelekezo ya wataalam wa kilimo ili kupata mazao mengi zaidi.Wamesisitiza kuchangamkia fursa ya kupima afya ya udongo wa mashamba yao zinazotolewa bure na wataalamu kutoka Halamshauri, ili kuhakikisha wanafanya kilimo chenye tija na kuwa serikali inahamasisha kilimo bora na chenye tija kupitia matumizi ya taarifa sahihi za udongo.
Hayo yamebainishwa na Katibu Tawala Wilaya ya Mpanda Geofrey Mwashitete katika hafla ya kukabidhi vyeti vya afya ya udongo kwa baadhi ya wakulima katika kijiji cha Imilamate kata ya Itenka ambapo ameleeza kuwa kupitia vyeti hivyo wakulima wanapaswa kufuata elimu inayotolewa na wataalamu ili kuweza kuvuna mazao mengi zaidi.
Wakulima katika Wilaya ya Nsimbo wamefanyiwa zoezi la kupima afya ya udongo katika mashamba yao, ambapo walipewa vyeti vinavyoonyesha hali ya udongo pamoja na mapendekezo ya kitaalamu kuhusu namna ya kuboresha uzalishaji wa mazao.
Zoezi hili, ambalo linafanyika bure, limeandaliwa kwa lengo la kuwasaidia wakulima kuelewa mahitaji halisi ya mashamba yao na kuboresha matumizi ya mbolea na virutubisho vya udongo. Vyeti vilivyotolewa vinaonyesha taarifa za kina kama vile kiwango cha asidi (pH), kiasi cha virutubisho vilivyopo, na mahitaji muhimu kwa ajili ya mazao yanayokusudiwa kulimwa.
Akisoma taarifa mbele ya mgeni rasimi Afisa Mazao wa wilaya Bwa. Rodrick Ntulo amesema kuwa Halmashauri ya Nsimbo kuanzia mwezi juni hadi kufikia tarehe 22 mwezi 11 mwaka huu wakulima 508 wamepimiwa afya ya udongo huku kata ya Itenka ikiwa na jumla ya wakulima 205 waliokuwa wamekwisha pimiwa mashamba yao.
Aidha, Afisa Kilimo wa Wilaya alibainisha kuwa kupima afya ya udongo ni hatua muhimu katika kuhakikisha kuwa wakulima wanatumia mbolea na mbinu za kilimo zinazofaa, huku wakiokoa gharama na kuhifadhi mazingira. "Kupima afya ya udongo ni mwanzo wa mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo. Tunawahimiza wakulima wote kutumia fursa hii," alisema.
Aidha alisisitiza na kuwahimiza wakulima kudai risiti kila wanaponunua mbegu na kuzitunza vizuri kwani zitasaidia kufuatilia malalamikao yao kwa urahisi. Alieleza hayo wakati akijibu swali la mkulima aliyeuliza juu ya hatua zitakazochukuliwa kwa wale wanaowauzia mbegu feki ambazo hupelekea hasara kubwa katika kilimo chao. Aidha alisema kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa juu ya ya wauzaji wa mbegu hizo feki ili kuhakikisha haki na uadilifu vinazingatiwa katiaka sekta ya kilimo.
Katibu Tawala wa wilaya ambae alimuwakilisha MKuu wa Wilaya ya Mpanda Mh Jamila Yusufu Kimaro, alitoa ufafanuzi kuwa serikali inaendelea na jitihada za kupunguza bei ya mbolea kwa kupitia ruzuku na mipango ya kuhakikisha inapatikana kwa urahisi na kwa bei nafuu. Aliyasema hayo wakati akirejea hoja iliyokua ikidai kua mbolea zipo juu kiasi kwamba wananchi wanashindwa kununua hivyo kushindwa kumudu kilimo chenye tija.
Akiendelea Kutoa ufafanuzi aliwasihi wakulima kufutilia kwa karibu maelekezo ya serikali kuhusiana usambazaji wa mbolea ya ruzuku na kuhakikisha wananunua kwa wauzaji waliothibitishwa ili kuepuka mbolea zisizo na ubora.
’’Tunatarajia kuwa na kikao na wadau wa Pembejeo ili kuzungumza nao hasa kuhusiana na bei na ubora wa mbolea amapo tutatoa majibu ya pamoja na hiyo ni baada ya kuwasikiliza na kutoa muongozo juu ya mbolea hizi’’
Katibu Tawala huyo alisisitiza Wakulima wengine kuhamasishwa ili kupima afya ya udongo kwa manufaa ya baadaye. ‘’Serikali na viongozi wa kilimo waendelee kusambaza elimu na huduma hii. Kutoa mafunzo zaidi Mafunzo kwa wakulima kuhusu tafsiri ya vyeti na matumizi sahihi ya mbolea na virutubisho.Ufuatiliaji Baada ya wakulima kupata ripoti, ni vyema kuwe na ufuatiliaji wa utekelezaji wa ushauri uliotolewa’’
Nae Diwani wa kata ya Itenka pia alihamasisha wakulima kushiriki kwa wingi katika zoezi hili, akiwakumbusha kuwa huduma hiyo ni bure endelevu na inapatikana kwa kila mkulima. hivyo kwa wale ambao hawajapimiwa udongo wafanye hivyo kwa mazao bora na mengi
Wakulima waliopimiwa afya ya udongo wameonyesha shukrani kwa zoezi hili, wakieleza kuwa vyeti walivyopokea vitawasaidia kuboresha uzalishaji wa mazao yao huku wengine wakiuliza maswali na ufafanuzi wa yeti hivyo ambapo walipata maelekezo jambo ambalo lilileta tija katika tukio hilo.
Akihitimisha Katibu Tawala wa wilaya amesema, hatua hii inalenga si tu kuongeza tija kwa wakulima wa Nsimbo, bali pia kulinda udongo dhidi ya uharibifu unaotokana na matumizi mabaya ya mbolea na virutubisho. Serikali inatarajia kuwafikia wakulima wengi zaidi katika wilaya hiyo kupitia uhamasishaji unaoendelea kufanyika.
Mpanda to Tabora road
Anuani ya Posta: P.O.Box 688 Mpanda
Simu : 025 295 5164
Simu: 025 295 5164
Barua pepe: ded@nsimbodc.go.tz
Hatimiliki@2016GWF.Haki zote zimehifadhiwa