Kaimu Mganga mkuu wa Halmashauri ya Nsimbo Dkt. Boniface Masaga amesema kwamba, wanafunzi ni kundi muhimu la kufikiwa kwani wao ni wazazi wa kesho, na hivyo ni mabalozi muhimu wa kuhamasisha lishe bora kwa wenzao na familia zao. Amebainisha kuwa afya bora ni msingi wa kujenga jamii yenye nguvu na inayoweza kukabiliana na changamoto za kiuchumi na kijamii. Vilevile ameeleza umuhimu wa lishe bora unavyoweza kuzalisha viongozi bora wenye kuweza kuhimili mikikimikiki ya maisha kwa ujumla
‘’Ukiwa na afya iliyozorota kwa kutokufuata lishe bora akili nayo hudumaa, sasa sio rahisi kufaya maamuzi kwani lishe ina uhusiano wa moja kwa moja na akili toka utotoni’’.
Ameyasema hayo wakati akifungua rasmi maadhimisho ya siku ya lishe yaliyofanyika katika shule ya Sekondari Nsimbo. Maadhimisho haya hufanyika kila mwaka mwishoni mwa mwezi Oktoba, lengo kuu likiwa ni kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa lishe bora katika kufikia malengo ya afya kwa wote.
Halmashauri ya Nsimbo imejipanga kuendelea kutoa elimu ya lishe bora kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla ili kuhakikisha kizazi kijacho kinakuwa na afya bora na uwezo wa kuchangia maendeleo ya nchi.
Maadhimisho yamehudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo wanafunzi, waalimu maafisa wa afya, na viongozi wa jamii. Kauli mbiu ya mwaka huu ikiwa ni "Mchongo ni Afya zingatia unachokula"
Amehimiza wanafunzi na wananchi wengine kuzingatia aina ya vyakula wanavyokula kwa sababu afya bora inategemea ulaji wa vyakula vyenye virutubisho sahihi. Ameeleza kuwa kama kauli mbiu inavyosema, tunapaswa kuchagua chakula chenye lishe bora ili kuepuka magonjwa yanayo sababishwa na lishe duni kama vile utapiamlo, uzito kupita kiasi, na magonjwa yasiyo ambukiza kama kisukari na shinikizo la damu. Kwa kuchagua vyakula vyenye virutubisho vinavyohitajika na kuepuka vyakula visivyo na faida kwa afya.
Aidha afisa lishe wa Halmashauri Bi.Jackline Kitomari amesisitiza umuhimu wa lishe bora katika maadhimisho hayo ya kitaifa, akiwahimiza wanafunzi pamoja na wananchi kuzingatia ulaji wenye virutubisho kamili ili kuboresha afya na maendeleo ya jamii. Vilevile ametoa wito kwa wazazi kuhakikisha watoto wao wanapata chakula chenye virutubisho sahihi kwa ajili ya ukuaji na maendeleo mazuri ya mwili na akili. Ameeleza kuwa lishe bora si tu suala la chakula, bali pia ni kipengele muhimu katika kujenga taifa lenye nguvu na uchumi imara.
Ameeleza kuwa lishe bora inahusisha vyakula kutoka makundi yote muhimu, yakiwemo wanga, protini, vitamini, madini, na mafuta. Amefafanua zaidi kwamba mwili unahitaji nguvu za kufanya kazi, ukuaji na ujenzi wa misuli,kujikinga na magonjwa na kuimarisha mifumo ya mwili pamojana afya ya ngozi na ubongo ameyasema haya wakati akielezea kila kundi la chakula na umuhimu wake katika mwili wa binadamu.
Aidha Waalimu wamezungumzia umuhimu wa lishe bora kwa maendeleo ya afya na akili za watoto na vijana, wamebainisha kuwa lishe bora ina mchango mkubwa katika uwezo wa kujifunza kwa watoto. Wameeleza kwamba, watoto wanaopata chakula chenye virutubisho kamili wana nguvu zaidi, wanaweza kuzingatia vizuri masomo yao, na kuwa na maendeleo mazuri kitaaluma. Pia wamesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wazazi na waalimu ili kuhakikisha watoto wanapata mlo bora nyumbani na shuleni kwa maendeleo yao ya kielimu na afya bora.
Kwa upande wa wanafunzi wamepata fursa ya kuuliza maswali na kushiriki katika mijadala kuhusu afya na lishe bora. Vilevile, wamefundishwa mbinu mbalimbali za kuandaa chakula chenye virutubisho sahihi na jinsi ya kujikinga dhidi ya magonjwa yanayosababishwa na lishe duni. Maonyesho ya vyakula vilivyoandaliwa kwa kuzingatia lishe bora yamefanyika, na kuwapa wanafunzi na waalimu nafasi ya kujifunza kwa vitendo
Pia wanafunzi wametoa shukrani zao kwa viongozi, waalimu, na wazazi kwa juhudi za kuwapatia lishe bora. Wameeleza kuwa lishe nzuri inawasaidia kuwa na nguvu, kuzingatia masomo, na kufanya vizuri darasani. Pia wamesisitiza kuwa wataendelea kujifunza kuhusu lishe bora na kushiriki katika mipango ya lishe shuleni na nyumbani ili kuboresha afya zao na kufikia malengo yao kitaaluma. Aidha wamesema kuwa watakua mabalozi wazuri kwa wanafunzi wenzao ambao hawakuwepo katika maadhimisho hayo.
Nao maafisa lishe wengine walio ongozana na mgeni rasmi wametoa elimu juu ya athari za lishe duni na jinsi inavyoweza kuathiri maendeleo ya watoto na uwezo wao wa kujifunza. Pia wametoa mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi na Waalimu kuhusu mbinu za kuandaa vyakula vyenye virutubisho vya kutosha, huku wakionyesha jinsi ya kuboresha mlo wa kila siku kwa kutumia malighafi zinazopatikana katika mazingira ya kawaida.
Katika kuimarisha ujumbe wa maadhimisho hayo, zoezi la upimaji wa afya lilifanyika ambapo wanafunzi na washiriki wengine wamepimwa uzito na urefu ili kubaini hali yao ya lishe. Kwa wale waliopungua uzito, wamepatiwa ushauri wa namna ya kuongeza virutubisho sahihi kwenye mlo wao ili kuboresha afya zao. Wale waliozidi uzito pia wameshauriwa kuhusu ulaji unaofaa na mazoezi ili kudhibiti uzito wao kwa njia bora.
Viongozi wametoa wito wa kuendelea na juhudi za kuboresha lishe ili kuijenga jamii yenye afya na uwezo wa kuchangia kikamilifu katika uchumi wa Taifa. Wamesema ni wazi kuwa lishe bora ni msingi wa ustawi wa jamii, na kwa pamoja, kila mmoja anahimizwa kuchukua hatua za kuboresha lishe kwa mustakabali bora wa watoto na taifa kwa ujumla.
Akihitimisha afisa lishe amesisitiza kuwa Maadhimisho haya yameonyesha umuhimu wa kila kundi la chakula katika kujenga jamii yenye afya na elimu bora. Kwa ushirikiano wa pande zote, jamii ina nafasi nzuri ya kufikia maendeleo endelevu kupitia lishe bora na virutubisho kamili.
Mpanda to Tabora road
Anuani ya Posta: P.O.Box 688 Mpanda
Simu : 025 295 5164
Simu: 025 295 5164
Barua pepe: ded@nsimbodc.go.tz
Hatimiliki@2016GWF.Haki zote zimehifadhiwa