Kuelekea uchaguzi mkuu unatarajia kufanyika Oktoba 29, 2025, wasimamizi wa vituo na wasimamizi wasaidizi katika vituo vya kupigia kura katika Jimbo la Nsimbo Mkoani Katavi wamepewa mafunzo elekezi ili kutekeleza majukumu yao kwa weledi.
Mafunzo hayo ya siku mbili yanayofanyika katika ukumbi wa shule ya Sekondari Nsimbo iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo yamefunguliwa leo na Msimamizi wa Uchaguzi katika Jimbo la Nsimbo Bwana Julius Zakaria Moshi ambapo amewataka washiriki wote katika semina hiyo kufuata sheria, kanuni, taratibu na miongozo inayotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Bwana Moshi amewakumbusha wasimamizi hao pamoja na wasimamizi wasaidizi katika vituo vya kupigia kura kufuatilia kwa umakini mafunzo yanayotolewa nawatendaji wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ili wawe watendaji wazuri na waendelee kuwa wazalendo, waaminifu na kufanya kazi kwa uadilifu kwa kufuata viapo vyao kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Aidha, Bwana Julius Moshi amewataka wasimamizi na wasimamizi wasaidizi katika vituo vyao kuepuka kuwa chanzo cha migogoro na vyama vya siasa kwa kuvishirikisha vyama hivyo kupitia mawakala wa vyama vyote vya siasa vyenye usajili kamili na vinavyoshiriki uchaguzi mkuu katika hatua zote kwa kuzingatia matakwa, sheria, kanuni na maelekezo mbalimbali ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Sambamba na hayo, Bwana Moshi amewataka wasimamizi na wasimamizi wasaidizi hao kusoma kwa makini Katiba, sheria, kanuni, miongozo na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na yanayotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ili kama kuna jambo lolote litawatatiza waweze kuuliza kwa watu sahihi na hatimaye kupata ufafanuzi wa jambo litakaloonekana kuwa na changamoto katika utekelezaji wa majukumu waliyopewa.
Kabla ya kufunguliwa kwa mafunzo hayo, Wasimamizi na wasimaizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya Kata wamekula kiapo cha kutunza siri na kujivua uanachama kwa waliokuwa wanachama wa vyama vya siasa kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na madiwani mwaka huu.
Katika Jimbo la Nsimbo jumla ya wapiga kura 108,819 wanatarajia kupiga katika vituo 281 vya kupigia kura.
Itakumbukwa kwamba, Tuma Huru ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza Siku ya Jumatano ya taerehe 29/10/2025 kuwa siku ya Uchaguzi mkuu, ambapo watanzania wenye sifa watatumia haki yao ya kikatiba ya kumchagua Rais, wabunge na madiwani watakaowaongoza kwa kipindi cha miaka mitano.
KURA YAKO HAKI YAKO, JITOKEZE KUPIGA KURA
Mpanda to Tabora road
Anuani ya Posta: P.O.Box 688 Mpanda
Simu : 025 295 5164
Simu: 025 295 5164
Barua pepe: ded@nsimbodc.go.tz
Hatimiliki@2016GWF.Haki zote zimehifadhiwa