Waziri wa Uchukuzi Mh. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (MB) akiwa ziarani Wilaya ya Mpanda ameweka jiwe la msingi katika miradi ya maendeleo inayoendelea katika Halmashauri ya Nsimbo kata ya Kanoge na Ugalla pamoja na kukagua marekebisho ya reli ya Kaliua kwenda Mpanda. Amefanya hayo mkoani Katavi wilaya ya Mpanda ikiwa ni moja ya ziara zake za kikazi ambapo alipata wasaa wa kuzungumza na wananchi kuhusiana na mambo mbali mbali.
Waziri ameanza ziara yake kwa kutembelea mradi wa ujenzi wa maji KABUGA - BULEMBO katika kijiji cha Kabuga kata ya Kanoge ambapo ameweka jiwe la msingi katika mradi huo. Mradi huu unalenga kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi kijiji cha Kabuga na Bulembo. Ameisisitiza kwamba, Serikali ya awamu ya sita inafanya juhudi kubwa kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi wake.
Aidha, baada ya kutembelea kijiji hicho, Waziri ameendelea na ziara yake katika kata ya Ugalla ambapo ameweka jiwe la msingi katika ujenzi wa mabweni mawili katika Shule ya Sekondari ya Ugalla River kwa ajili ya wanafunzi wa kike na wa kiume, ambapo yamekadiriwa kubeba wanafunzi 80. Akiwa shuleni hapo, Waziri ameweka jiwe la msingi la mradi huo wenye thamani ya shilingi 200,000,000 (milioni mia mbili). Pamoja na shughuli hiyo, amewahimiza wanafunzi kusoma kwani fursa haiji mara mbili. Amewataka kupambana kimasomo kwa kuwa changamoto ni nyingi lakini pia fursa ni nyingi hivyo wasiogope kupambana. Amesema kwamba Elimu ndiyo msingi wa maendeleo na mafanikio yao ya baadaye.
Baada ya hapo Waziri ametembelea reli ya kutoka Kaliua kwenda Mpanda ambayo kwa sasa inafanyiwa marekebisho ili kuboresha usafiri wa reli katika eneo hilo. Katika ukaguzi huo, alitumia kiberenge kwa ajili ya kukagua ubora wa njia na hatua zinazochukuliwa kuboresha reli hiyo ambayo ina umuhimu mkubwa kwa usafiri wa mizigo na abiria.
Waziri Mbarawa ameeleza kuwa maboresho yanayoendelea kwenye reli hiyo yatachangia kupunguza muda wa safari kwani baada ya maboresho hayo, reli hiyo itakuwa na uwezo wa kusafiri kwa kasi ya kilometa 70 ikilinganishwa na kasi ya sasa ya kilomita 30 kwa saa. Aidha, amewahimiza wakandarasi wa reli hiyo kuzingatia ajira za wenyeji kwa kuwapa kazi ambazo wanazimudu ili kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa wakazi wa eneo hilo.
Waziri ameendelea kwa kumpongeza Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa mapenzi mema aliyonayo kwa wananchi kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo inayogusa wananchi moja kwa moja. Amewaomba wananchi kuendelea kumuombea dua njema ili aweze kuwahudumia zaidi. Pia, alimpongeza Mh. Mbunge Anna Lupembe kwa kuchapa kazi na kujituma kuchangia maendeleo yanayoonekana katika jimbo la Nsimbo ambapo aliwaomba wanachi kuendelea kumuumga mkono.
Amesema kuwa atahakikisha anafuatilia kwa ukaribu wale wanaofanya kazi katika reli hiyo kama vibarua wanalipwa stahiki zao kwa wakati na kuwa atasimamia kuona kila mmoja anapata haki yake. Alisema hayo wakati akijibu ombi la Mbunge Anna Lupembe lililomtaka kushughulikua vibarua ili waweze kulipwa kwa wakati na pia kuzingatiwa kulingana na kazi kubwa wanazozifanya.
Naye mkuu wa Mkoa wa Katavi Mh. Mwanamvua Hoza Mrindoko alisema kuwa Serikali ya awamu ya sita imeleta mapinduzi makubwa na kuwa tumepokea pesa kiasi cha trillion 1.3 kwa ajili ya miradi ambayo kila sekta zimefikiwa. Alisema hayo akimkaribisha waziri wa uchukuzi ili aweze kuzungumza na wananchi.
Katika ziara hiyo Waziri ameambatana na viongozi mbalimbali wakiwepo Mbunge wa Jimbo la Nsimbo, Mkuu wa Wilaya, Katibu Mkuu, mwenyekiti wa halmashauri ya Nsimbo viongozi wa chama, na viongozi wengine wengi. Kila kiongozi aliyeshiriki aliwasilisha shukrani kwa Rais kwa kuendelea kufadhili miradi mingi yenye manufaa kwa wananchi wa Katavi na kupeleka fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Mwenyekiti wa Halmashauri pia alitoa shukrani zake na kusema kuwa miradi hii inachangia sana katika kuboresha maisha ya wananchi.
Mwisho wa mkutano, Waziri aliwakumbusha wananchi umuhimu wa kushiriki katika zoezi la uchaguzi. Aliwahimiza wale ambao wamejiandikisha kuhakikisha wanajitokeza kupiga kura ili kutumia haki yao ya kidemokrasia na kuchagua viongozi watakaowawakilisha vizuri.
Ziara hii imeacha taswira chanya kwa wananchi, huku Waziri akionesha dhamira ya Serikali katika kuendelea kuimarisha miundombinu na huduma za kijamii kwa ajili ya ustawi wa wananchi wa Mkoa wa Katavi.
Mpanda to Tabora road
Anuani ya Posta: P.O.Box 688 Mpanda
Simu : 025 295 5164
Simu: 025 295 5164
Barua pepe: ded@nsimbodc.go.tz
Hatimiliki@2016GWF.Haki zote zimehifadhiwa